IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Utawala wa Kizayuni hauna uhalali, utaangamia kwa hima ya mataifa ya Waislamu

20:53 - June 15, 2018
Habari ID: 3471560
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Tatizo la utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuwa hauna uhalali, ni utawala ambao msingi wa uundwaji wake ni batili, kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu na kwa hima ya mataifa ya Waislamu, utawala huo kwa yakini utaangamia."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran katika Baraza la Idul Fitr ambalo limewaleta pamoja viongozi wa ngazi za juu nchini, wananchi wa matabaka mbali mbali na mabalozi wa nchi za Kiislamu. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema moja ya sababu muhimu zaidi za kupelekea kuheshimiwa jamii za Kiislamu duniani ni umoja na kutatua hitilafu zilizopo.

Ameongeza kuwa, leo madola ya kiistikbari yanaibua hitilafu na misuguano baina ya Waislamu katika umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Njia pekee ya kukabiliana na sera hizi za Wamarekani watenda jinai na Wazayuni ni kufahamu ipasavyo njama za adui na kusimama kidete kukabiliana nazo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema viongozi wa kisiasa, kidini na kiutamaduni katika umma wa Kislamu wana jukumu zito katika kuyasaidia mataifa kukabiliana na madola ya kiistikbari. Huku akiashiria kuhusu malengo ya kuundwa utawala bandia wa Israel katika eneo amesema: "Moja ya malengo asili ya kuasisiwa utawala huu ni kuleta hitilafu baina ya mataifa ya Waislamu." Hata hivyo amesema uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni unakabiliana na mgogoro wa utambulisha na hivyo utawala huo hautadumu.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa hatua ya baadhi ya tawala zenye mitazamo dhaifu katika eneo kuanzisha uhusiano wa siri na wa wazi wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni pamoja na hatua ya Marekani kuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds ni hatua ambazo haziwezi kuusaidia  utawala wa Kizayuni. Amesema utawala huo wa Kizayuni umejengeka katika msingi wa mabavu, vitisho na mauaji pamoja na kulitimua taifa katika ardhi yake na kwa msingi huo, utawala wa Kizayuni hauna uhalali wowote miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa haiyumkiniki kuifuta nafasi ya Palestina katika kumbukumbu  ya kijiografia na kihistoria duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine amesisitiza ulazima wa kufanyika kura ya maoni itakayohusisha Wapalestina halisi, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Mayahudi ili kuamua mfumo wa utawala Palestina na kuongeza kuwa: "Kufanyika kura kama hii ya maoni na kuundwa serikali ya Palestina kwa kutegemea kura za Wapalestina kwa hakika kuna maana ya kuangamizwa utawala bandia wa Israel na kwa yakini hili litaweza kufanyika katika mustakabali usio mbali."

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kuangamizwa utawala wa Kizayuni kutaleta umoja na izza katika umma wa Kiislamu.

Marekani imeshindwa katika eneo

Wakati huo huo mapema leo asubuhi, Kiongozi Muadhamu ameyasema aliswalisha Swala ya Idul Fitr mjini Tehran na katika hotuba za baada ya swala aliashiria siasa za Rais Donald Trump wa Marekani katika eneo hili amesema: "Rais wa Marekani alisema kuwa, nchi yake imetumia kiasi cha Dola trilioni saba katika eneo la Mashariki ya Kati, suala ambalo linaashiria kushindwa Marekani katika eneo hili,  kwa kuwa kadri wanavyotoa fedha zao hawatopata faida yoyote."

Utawala wa Kizayuni hauna uhalali, utaangamia kwa hima ya mataifa ya Waislamu

Kadhalika katoka hotuba hiyo, Ayatullah Khamenei amegusia njama mbalimbali za maadui ikiwemo ya kuliwekea mashinikizo taifa la Iran na amesisitiza umuhimu wa kudumishwa umoja na mshikamano kati ya viongozi, wananchi na weledi kwa ajili ya kukabiliana na njama hizo.

Aidha alizungumzia ushiriki mkubwa wa wananchi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kusema, ushiriki watu katika maandamano ya siku hiyo ulikuwa mkubwa zaidi kuliko mwaka uliopita na kwamba siasa za kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinazidi kulifanya taifa hili lichanue na kuimarika siku baada ya siku. Amesisitiza kwamba mataifa ya ulimwengu wa Kiislamu yamebaini kwamba, Siku ya Kimataifa ya Quds ni kwa ajili ya kulisaidia taifa la Palestina na kwamba siku hiyo imeendelea kuenziwa katika nchi nyingi za dunia licha ya propaganda nyingi za kutaka kupotosha malengo ya siku hiyo.

Kiongozi Muadhamu alibaini kuwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni medani ya mashindano ya kumtii Mwenyezi Muungu na kupata ridhaa zake baina ya waumini na siku ya Idi ni uwanja wa kupewa malipo na tuzo.

3708800/

captcha