IQNA

Misri yawaweka wanachama zaidi ya 100 wa Ikhanul Muslimin katika orodha ya magaidi

22:06 - April 12, 2021
Habari ID: 3473806
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Misri imewaweka wanachama wengine 103 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin kwenye orodha ya magaidi kufuatia hukumu zilizotolewa na mahakama za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa, mnamo tarehe 9 Machi na tarehe 4 Aprili mwaka huu, vyombo vya mahakama vya Misri vilitoa jumla ya hukumu nane kwa watu 103 ambao ni wanachama wa Ikhwanul Muslimin na kuongeza kuwa, kitengo cha kupambana na utakatishaji pesa na kuudhamini kifedha ugaidi cha Misri kimeyaweka majina ya watu yanayoonekana kwenye tovuti ya kitengo hicho, kwenye orodha ya magaidi.

Tangu tarehe Julai 2016 hadi tarehe Aprili 2021, jumla ya watu 6,761, yamewekwa kwenye orodha ya magaidi.

Maafisa wa vyombo vya mahakama vya Misri wanadai kuwa, imethibitika rasmi kwamba watu hao wamehusika katika jinai za kigaidi ndani ya nchi hiyo na baadhi yao wamesaidia kufadhili kifedha na kuwapatia silaha watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka ili wazitumie dhidi ya wananchi.

Mwaka 2013, baraza la mawaziri la Misri liliitangaza rasmi harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Julai 3 2013 yaliyoongozwa na waziri wa ulinzi wakati huo Jenerali Abdel Fattah el Sisi kumuondoa madarakani marehemu rais Muhammad Morsi, machafuko yaliongezeka nchini humo na mapigano makali yakaigubika Misri baina ya wafuasi wa kiongozi huyo na vikosi vya usalama vya serikali ya mapinduzi.

Mamia ya watu wameuawa na maelfu wametiwa nguvuni katika mapigano hayo.

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ilikutangaza kuondolewa Morsi madarakani kuwa ni mapinduzi ya kijeshi, ambapo mbali na kuyalaani ilitaka kiongozi huyo arejeshwe madarakani.

Baada ya matukio yaliyojiri mwaka 2014 nchini Misri, Saudi Arabia na baadaye Imarati nazo pia ziliiweka Ikhwanul Muslimin kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.

3474437

captcha