IQNA

Rais Hassan Rouhani

Urutubishaji wa hadi kiwango cha asilimia 60 ni jibu kwa shari za maadui

18:14 - April 14, 2021
Habari ID: 3473813
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa urutubishaji wa madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 60 ni jibu kwa vitendo vya shari vya maadui.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumatano katika kikao cha baraza la mawaziri ambapo amesema hatua ya Iran kuanza kutumia mashinepewa au sentrifuji za kisasa aina ya IR-6 na urutubishaji wa madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 60 ni jibu muafaka kwa vitendo vya shari vya maadui. Ameongeza kuwa, iwapo Wazayuni wametekeleza njama dhidi ya Iran, basi tutatoa jibu na hilo ndio jibu la kwanza.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, hilo ni jibu kwa ukhabiti wa Wazayuni ili wafahamu kuwa hawawezi kupanga njama dhidi ya taifa la Iran na kutenda jinai katika kituo cha nyuklia cha Natanz.

Rais wa Iran alikuwa akishiria tukio la hivi karibuni la uharibifu uliofanywa katika kituo cha nyuklia cha Natanz kati mwa Iran Alhamisi iliyopita. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipiza kisasi kwa wakati mwafaka kutokana na uharibifu uliofanywa na Israel katika kituo hicho cha Natanz.

Kwingineko Rais Rouhani ameongeza kuwa: "Tutakata mikono ya Wazayuni wanapotenda jinai." Aidha amesema Iran itashinda katika vita vya kiuchumi na hatimaye dhulma itafika ukingoni.

Halikadhalika Rais wa  Iran ameendelea kusema kuwa, wale ambao wameyachukua mateka maisha ya watu na kutatiza jitihada za Iran za kupata chanjo na vyakula wafahamu kuwa lazima mikono yao lazima itakatwa.

Rais Rouhani ametoa shukrani zake za dhati kwa sekta ya afya nchini Iran na kusema sekta hiyo ina  jukumu nzito sana wakati huu wa janga la corona.

Kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, Rais Rouhani amesema Marekani lazima irejee katika mapatano hayo kama ilivyokuwa wakati yalipofikiwa mwaka 2015. Amesema Iran imetangaza bayana kuwa pale Marekani itakapochukua hatua za kivitendo za kutekeleza ahadi zake, Iran nayo iatrejea katika kutekeleza ahadi zake za mapatano ya JCPOA.

3964445

captcha