IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mazungumzo ya JCPOA yasiwe marefu kupita kiasi, sera za Iran ziko wazi

22:36 - April 14, 2021
Habari ID: 3473814
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumza kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na vikwazo na kusema sera za Iran ziko wazi kuhusu JCPOA na vikwazo. Ameongeza kuwa sera hizo amezibainisha wazi kwa wakuu wa nchi kupitia maandishi na katika mikutano.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatano jioni mjini Tehran wakati akiwahutubia kwa njia ya video washiriki wa mahafali ya kuwa na ukuruba na Qur'ani Tukufu iliyofanyika katika siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini (MA).
Kiongozi Muadhamu amesema, wakuu wa nchi wameamua kuenda kufanya mazungumzo ili sera hizo zitekelezwe na kuongeza kuwa ingawa hapingi suala hilo lakini kuna ulazima wa kuchukua tahadhari ili kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo hayaendelei kwa muda mrefu kupita kiasi kwani hilo litakuwa kwa madhara ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, lengo la Wamarekani katika kusisitiza kuhusu mazungumzo ni kutaka kulazimisha kauli batili na kuongeza kuwa: "Mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, awali kabisa Marekani inapaswa kuondoa vikwazo kwani (Wamarekani) hawaaminiki. Huko nyuma walikiuka ahadi zao mara kadhaa kiasi kwamba hata baadhi ya washiriki katika mazungumzo kutoka Ulaya wanakiri hilo katika vikao vya faragha ingawa wakati wa kuchukua maamuzi wanajisalimisha kwa Wamarekani na hawawezi kuchukua maamuzi huru."
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa,"Mapendekezo ya Wamarekani huwa yamejaa kiburi na ni ya udhalilishaji kiasi kwamba hayawezi kutazmwa. Ni matumaini yetu kuwa, wakuu wa serikali nchini Iran watasonga mbele wakiwa waangalifu, kwa ukakamavu na kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kwa dhikri ya Hasbunallah wa neema al wakil na hivyo kwamba kwa taufiki na uwezo wake Mwenyezi Mungu wataweza kulifurahisha taifa."
Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito kwa Waislamu kusoma Qur'ani Tukufu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na pia wazingatia kuhusu aya wanazosoma. Aidha amewataka maqarii wa Qur'ani Tukufukuwa ni wahubiri wa Kitabu hicho kitakatifu na hivyo qiraa yao inapaswa kuandamana na unyenyekevi na kuzingatia maana ya aya wanazosoma.

3964657

captcha