IQNA

Waislamu Uingereza

Wanafunzi watembelea Msikiti nchini Uingereza kujifunza Uislamu

19:59 - December 02, 2022
Habari ID: 3476183
TEHRAN (IQNA) – Wanafunzi kutoka shule ya Darwen walitembelea Msikiti wa Madina mjini Blackburn Uingereza ili kujua zaidi kuhusu Uislamu na maisha ya kila siku ya Waislamu.

Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kozi ya Uraia ya GCSE inayofundishwa katika Shule ya Darwen Aldridge Enterprise Studio (DAES).

Wanafunzi katika darasa za 9, 10 na 11 walikaribishwa na mwalimu mkuu wa madrassah ya msikiti, Maulana Abbas ambaye aliwatembeza katika msikiti huo, ambao uko katika mtaa wa Oak.

Pia kulikuwa na usomaji wa baadhi ya mashairi ya Kiislamu, fasihi, na Qur’ani katika mjumuiko huo. Mwishoni mwa ziara hiyo, wanafunzi walialikwa na Imamu kushiriki katika kipindi cha maswali na majibu na baadaye wakala chakula kilichoandaliwa na mwalimu wa sayansi Bw Hussain.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa baadhi ya wanafunzi kuingia ndani ya msikiti.

Mwalimu wa somo la uraia Bi Arnone alisema: "Safari nzima kwangu ilikuwa njia nzuri ya kuujua utamaduni na maarifa ya imani ya Kiislamu.

"Safari ya msikiti ilikuwa nzuri na Imam aalikuwa wa kirafiki sana, na ilikuwa ni furaha kuona wanafunzi wetu wakishiriki katika mchakato huo."

"Msikiti ulikuwa mahali pa kukaribisha sana tangu tulipoingia hadi tulipotoka. Sote tulivutiwa na uzuri wa vyumba vya kuswalia na elimu inayofanyika msikitini.

"Tuliondoka tukiwa tumeimarishwa na uzoefu tuliopata. Imam aliwatia moyo wanafunzi kufikiria kuhusu tamaduni na imani nyingine na alizungumza kwa uwazi kuhusu imani yake na safari yake ya kuwa Imam.

"Kwa ujumla, hili lilikuwa tukio ambalo ningependekeza kwa mtu yeyote bila kujali ni wa imani gani."

Maulana Abbas alisema: “Nilifurahia sana kutumia muda na wanafunzi na walimu. Walikuwa na muamala mzuri.”

"Wanafunzi wote walikuwa na heshima sana na hiyo ni sifa kwa shule yao. Walimu wanafanya kazi nzuri sana na ninatumai tunaweza kuwa na matukio mengi zaidi kama haya yaliyoandaliwa kwa ajili ya kila mtu. Hongera kwa wote waliohusika."

Mkuu wa Shule, Colin Grand alisema: "Hii imekuwa fursa nzuri kwa wanafunzi wetu kukuza ujuzi wao wa kiutamaduni na ningependa kuwashukuru wote waliohusika kwa tukio hili liwe lenye kubakia katika kumbukumbu.”

"Tunajivunia kuwaendeleza wanafunzi wetu zaidi ya kile tunachofundisha darasani na ziara kama hii inakamilisha mtaala na kukuza vijana wetu na maarifa yao mapana.

"Tunatazamia kuendeleza ushirikiano zaidi na Msikiti wa Madina kwa fursa za siku zijazo.

"Tunapenda kuwashukuru wanakamati wote wa Msikiti wa Madina na watu waliojitolea kwa kuwaruhusu wanafunzi na walimu kutoka Shule ya  Darwen Aldridge Enterprise Studio kutembelea msikiti na kuongeza ufahamu wa umuhimu wa kukuza mshikamano wa jamii wa imani tofauti ili kila mtu apate uzoefu."

3481485

captcha