IQNA

Mashindano ya Qur'ani Tukufu

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran: Awamu ya kwanza yahitimishwa

16:10 - January 18, 2023
Habari ID: 3476425
TEHRAN (IQNA) - Mchakato wa tathmini katika duru ya mchujo ya Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran ilihitimishwa Jumanne.

Jopo la majaji katika vitengo vya  wanaume na wanawake katika mashindano hayo hivi karibuni litawataja wagombeaji ambao wamefuzu kwa fainali hizo.

Majaji walisikiliza klipu zilizorekodiwa na  kutumwa na washiriki katika mji mtakatifu wa Mashhad kaskazini mwa Iran mnamo Januari 13.

Jumla ya wasomaji na wahifadhi wa Qur'ani Tukufu 149 kutoka nchi 80 wakiwemo wanaume 114 na wanawake 35 walishiriki katika duru ya kwanza.

Jopo la majaji katika sehemu ya wanaume lilijumuisha wataalamu wa Qur'ani Tukufu wa Iran kama Nusratullah Husseini, Reza Mohammadpour, Saeed Fayaz, Hamid Derayati na Mohammad Sadeq Nasrullahi.

Pia kulikuwa na wataalamu wawili wa kigeni, Seyed Ahmad Ghaffari kutoka Afghanistan na Ahmed Abdulbari kutoka Iraq, waliokuwa wakihudumu katika jopo hilo lililokuwa likiongozwa na Seyed Ali Sarabi.

Hatua ya mwisho katika sehemu za wanaume na wanawake imepangwa kuanza tarehe 13 Februari, sambamba na Siku ya Maba’ath (kuashiria kuteuliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kama mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu).

Kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni kama ya mwaka jana ambayo ni, "Kitabu Kimoja, Umma Mmoja", nukta ambayo inaashiria umuhimu wa umoja na mashikamano wa Waislamu katika sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la Wakfu na Misaada la Iran kila mwaka huandaa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani kwa kushirikisha wanaharakati wa Qur'ani kutoka nchi mbalimbali.

4115396

captcha