IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Kiongozi wa Kishia Bahrain: Kuvunjiwa heshima Qur’ani hakuna uhusiano wowote na uhuru wa maoni

10:29 - January 26, 2023
Habari ID: 3476466
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini wa Bahrain Sheikh Isa Qassim amelaani vikali kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu hivi karibuni katika nchi za Ulaya.

Sheikh Qassim alisema katika taarifa yake kwamba, "Kitendo cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kilichotekelezwa na mtu mwenye msimamo mkali, anayejulikana kama Rasmus Paludan - kiongozi wa Chama cha Stram Kurs (Msimamo Mkali), chini ya ulinzi wa polisi na kwa ruhusa kutoka kwa serikali, nje ya ubalozi wa Uturuki huko Stockholm hakiwezi kuonekana kama uhalifu wa mtu binafsi bali ni kosa la kiserikali,”.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kipuuzi inaashiria kiwango cha kukata tamaa cha Paludan na serikali ya Uswidi, na kwamba jinai zote zinazofanywa katika baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya matukufu na thamani za Kiislamu ni za aina moja.

Sheikh Qassim alibainisha kwamba, "Itakuwa ni wazimu kuhesabu mashambulio mabaya kama haya dhidi ya maadili ya kidini kama uhuru wa mawazo na maoni. Waanzilishi na wafadhili wake wana imani kwamba kama wanyama wengine, wanadamu wanaruhusiwa kufanya au kupata chochote wanachotaka."

Msomi huyo mashuhuri wa Kishia wa Bahrain aliendelea kusisitiza kwamba matusi, uwongo, kashfa, unafiki na kuvunjiwa heshima maadili matukufu hayawezi kwa vyovyote vile kuzingatiwa kuwa ni uhuru wa maoni.

Amesisitiza nukta hiyo kwa kuhoji, "Ni kwa nini hawaruhusu chuki dhidi ya Wayahudi, au kukanwa kwa mauaji ya Wayahudi (Holocaust)  na kuchomwa moto bendera za watu wenye uhusiano wa jinsia moja? Je, hatua hizo nao haziweki mipaka uhuru wa kibinafsi?”

Aidha amesema vitendo vya kuvunjia heshima matukufu ya Kiisalmu katika nchi za Magharibi, kama vile ulivyofanyika Jumamosi mbele ya macho ya zaidi ya watu bilioni moja na huku kukiwa na ukimya na uungwaji mkono wa serikali za Ulaya, unaonyesha wazi nia ovu ya kuleta uasi na machafuko duniani kote na kudhoofisha usalama ulimwengu ulimwenguni

Sheikh Isa Qassim  ametoa wito kwa wasomi kuchukua hatua za kuzuia vitendo kama hivyo , ambayo vitasababisha kuenea kwa ugaidi bila kizuizi. Aidha amesema, kwa ajili ya amani na utulivu duniani, wasomi wanapaswa kulaani vikali vitendo hivyo vya kuvunjiwa ehsima Qur'ani Tukufu.

Siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu  huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Uchochezi huo mpya ulifuatia kitendo sawa na hicho cha chuki dhidi ya Uislamu siku ya Jumamosi nchini Uswidi, ambapo mtu mwenye msimamo mkali  raia wa Denmark alichoma nakala ya Qur’ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidhinishwa na kusimamiwa na polisi nchini humo.

3482207

captcha