IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu / 59

Uvunjaji wa Ahadi wa Mayahudi Kama Ilivyofafanuliwa katika Sura Al-Hashr

17:30 - January 29, 2023
Habari ID: 3476480
TEHRAN (IQNA) – Baada ya Waislamu kuhama au kugura kutoka Makka kwenda Madina, makundi ya Wayahudi waliokuwa wakiishi katika mji huo walishirikiana na Waislamu, wakiahidi kuwaunga mkono endapo vita vitatokea.

Hata hivyo, makundi ya Kiyahudi yalikiuka ahadi yao na kuwasaidia maadui wa Waislamu na hili likapelekea kufukuzwa kwao kutoka Madina. Haya yametajwa katika Sura Al-Hashr.

Al-Hashr ni sura ya 59 ya Qur'ani Tukufu ambayo ina aya 24 na iko katika Juzuu ya 28. Ni Madani na ni Sura ya 101 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Hashr kwa Kiarabu ina maana ya kuwafukuza watu kutoka nyumbani kwao ili washiriki vitani, n.k. Aya ya 2 ya Sura inahusu kuwafukuza Wayahudi wa Bani Nadhir kutoka Madina.

Walikuwa kabila la Waarabu la Kiyahudi lililoishi kaskazini mwa Arabia kwenye oasis ya Madina hadi karne ya 7. Wakati Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na Waislamu walipokwenda Madina (inayojulikana kama Hijra), kabila la Bani Nadhir liliahidi kuwaunga mkono Waislamu na kuulinda mji pamoja nao endapo kutatokea mashambulizi ya adui.

Lakini walivunja ahadi yao na, kwa hiyo, kulikuwa na vita kati yao na Waislamu ambapo walishindwa na kufukuzwa Madina.

Maudhui ya Sura Al-Hashr hasa yanahusu kuanzishwa kwa majina na sifa za Mwenyezi Mungu, kanuni za vita, hatari ya Mayahudi na wanafiki na njama zao za pamoja dhidi ya Uislamu, matokeo ya kumsahau Mwenyezi Mungu, Tasbihi au viumbe vyote vinavymtukuza Mwenyezi Mungu , na nafasi ya Qur'ani Tukufu katika kuitakasa nafsi ya mtu.

Sura imeanza kwa Tasbihi na kumtukuza Mwenyezi Mungu: “Vinamsabihi, Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima..”

Kisha kunatajwa vita kati ya Waislamu wa Madina na Mayahudi waliovunja ahadi yao. Kwa mujibu wa aya hizo, hakuna aliyedhania kuwa Waislamu walikuwa na uwezo wa kuwashinda Mayahudi lakini Mwenyezi Mungu “alitia hofu katika nyoyo zao hata nyumba zao zikaharibiwa kwa mikono yao wenyewe”.

Kisha sura inajadili sheria kuhusu usambazaji wa ngawira za vita.

Pia inawakosoa wanafiki na kufichua tabia zao za uhaini dhidi ya Waislamu.

Vile vile katika sehemu fupi, aya hizo zinatoa maelezo ya Quran Tukufu na athari zake katika utakaso wa nafsi. Kisha Sura inataja baadhi ya sifa za Mwenyezi Mungu na Asma al-Husna Wake (majina mazuri).

captcha