IQNA

Muhyiddin Yassin ateuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Malaysia

18:51 - February 29, 2020
Habari ID: 3472516
TEHRAN (IQNA) - Mfalme wa Malaysia amemteua Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa nchi hiyo, Muhyiddin Yassin kuwa Waziri Mkuu mpya, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mahathir Muhammad, ambaye alijiuzulu hivi karibuni.

Taarifa kutoka Kasri la Mfalme wa Malaysia imesema, Mfalme amemteua Muhyiddin kwa msingi kuwa, ana uungaji mkono mkubwa bungeni. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Mfalme ametoa dikrii inayosema kwamba mchakato wa kumteua Waziri Mkuu hauwezi kucheleweshwe zaidi. Huu ni uamuzi muafaka na bora kwa wote."

Muhyiddin mwenye umri wa miaka 72 na ambaye anatazamiwa kuapishwa kesho Jumapili amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa, "nawaomba Wamalaysia wote wakubali uamuzi huo wa Mfalme."

Chama tawala cha UMNO ambacho kiko madarakani kwa miongo sita sasa pamoja na chama cha Kiislamu cha PAS ni katika vyama ambavyo vilikuwa vinamuunga mkono Muhyiddin.

Haya yanajiri katika hali ambayo, mapema leo Muungano wa Tumaini (Alliance of Hope) ukiongozwa na hasimu na mpinzani wa kisiasa wa muda mrefu wa Dakta Mahathir, Anwar Ibrahim umetangaza kuwa unamuunga mkono kikamilifu mwanasiasa huyo kushika tena wadhifa wa uwaziri mkuu wa nchi hiyo.

Mahathir, mwenye umri wa miaka 94, kwa ushirikiano na Ibrahim mwenye umri wa miaka 72 walifanikisha ushindi wa Muungano wa Tumaini uliowashangaza wengi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018; lakini misuguano ya kisiasa baina yao imeendelea kushuhudiwa na ndiyo iliyokuwa chanzo cha mgogoro wa kisiasa uliozuka nchini Malaysia hivi karibuni na kupelekea kujiuzulu Mahathir Muhammad.

3470778

 

captcha