IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani inahamishia magaidi wa ISIS Afghanistan ili kuhalalisha uwepo wake katika eneo

13:30 - January 30, 2018
Habari ID: 3471376
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kuuawa watu wasio na hatia katika hujuma za hivi karibuni za kigaidi nchini Afganistan na kusema: "Lengo la Marekani katika kuhamishia Afghanistan magaidi wa ISIS (Daesh) ni kuhalalisha uwepo wake katika eneo sambamba na kudhamini usalama wa utawala wa Kizayuni."

Marekani inahamishia magaidi wa ISIS Afghanistan ili kuhalalisha uwepo wake katika eneoAyatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran katika mwanzo wa darsa yake ya kharij (masomo ya juu kabisa) katika taaluma ya fiqhi. Ameashiria kuwepo nyayo za ISIS katika ugaidi wa hivi karibuni Afghanistan ambapo mamia ya watu wameuawa na kuongeza kuwa: "Wale walioanzisha ISIS na kutumia kundi hilo kama chombo cha kueneza udhalimu na jinai dhidi ya watu Syria na Iraq, sasa baada ya kushindwa katika nchi hizo wanahamishia ISIS nchini Afghanistan na mauaji ya hivi karibuni ni mwanzo wa njama hiyo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Magaidi wanaopata himaya ya Marekani, hawatafautishi baina ya Shia na Sunni na wanawaua raia wawe ni Sunni au Shia."

Ayatullah Khamenei amesema sera inayopewa kipaumbele na Marekani ni kuyagonganisha mataifa ya eneo ili yajishughulishe na suala hilo. Ameongeza kuwa: "Marekani inataka kuhakikisha kuwa eneo hilo halishuhudii neema na serikali na mataifa ya eneo yajishughulishe na migongano baina yao ili yasifikirie kukabiliana na wakala khabithi wa uistikbari yaani, Uzayuni."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha zaidi kuhusu lengo la  Marekani katika kuibua machafuko katika eneo ili kuhalalisha kuendelea kubakia vikosi vyake katika eneo na kusema: "Wamarekani ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa amani Afghanistan; mauaji yanayotekelezwa kwa jina la dini katika eneo kwa karibu miaka 20 sasa yanachochewa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na vibaraka wa Marekani. Hivi sasa pia kwa kuibua ghasia na machafuko, wanataka kudhamini kuendelea kubakia kwao nchini humo ili kutekeleza malengo yao ya kisiasa na kiuchumi."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Laana ya Mwenyezi Mungu itawashukia waistikbari na vibakara wao pamoja na utawala khabithi na utendao jinai wa Kizayuni na Marekani kutokana na namna wanavyowaangamiza Waislamu."

3686681

captcha