IQNA

Lengo la utawala wa Kizayuni katika kuuchoma moto Msikiti wa Al Aqsa

17:15 - August 21, 2015
Habari ID: 3349544
Kutokana na pendekezo lililotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa ajili ya kuenzi Msikiti wa kihistoria wa al Aqsa, tarehe 21 Agosti imetangazwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Msikiti.

Kwa mnasaba huo Rais Hassan Rouhani alisema katika mkutano wa 13 wa Siku ya Kimataifa ya Msikiti kwamba kuchomwa moto Msikiti wa al Aqsa ni kielelezo cha utambulisho wa utawala wa kigaidi na kivamizi wa Israel. Rais Rouhani ameashiria tukio chungu la kuchomwa moto Msikiti wa al Aqsa katika siku kama hii ya leo hapo mwaka 1969 na kusema: Waislamu kamwe hawatasahau tukio chungu la kuchomwa moto kibla chao cha kwanza kulikofanywa na Wazayuni miaka 46 iliyopita na kwamba tukio hilo limeonesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel haujali wala kuheshimu msingi wowote wa kijamii au wa kibinadamu.

Siku ya Kimataifa ya Msikiti huadhimishwa kila mwaka nchini Iran na katika baadhi ya nchi duniani ili kukumbuka tukio la kuchomwa moto Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Mwaka 1969 Mzayuni Michael Dennis Rohan aliuteketeza kwa moto msikiti huo. Wakati huo maafisa wa Israel walitangaza kuwa mtu huyo aliyekuwa na uraia wa Australia, ni Mkisto mwendawazimu, lakini baadaye ilibainika kuwa Dennis Rohan ni Myahudi mwenye misimamo ya kuchupa mipaka na alichoma moto kibla hicho cha kwanza cha Waislamu kwa makusudi. Mbali na hayo ushahidi ulionesha kuwa Wazayuni wengine wenye misimamo mikali walimsaidia Michael Dennis Rohan katika harakati zake za kuchoma msikiti huo.

Quds na maeneo yake matakatifu yamekuwa yakishambuliwa na kuvunjiwa heshima tangu Wazayuni walipovamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita utawala wa kikatili wa Israel si tu kwamba hauwaonei huruma watoto wadogo na wanawake na umekuwa ukifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali pia umekuwa ukivunja na kuhujumu misikiti na makanisa ya eneo hilo. Pamoja na hayo Msikiti wa al Aqsa ndio unaoshambuliwa na kuvunjiwa heshima zaidi kati ya maeneo yote matakatifu ya Palestina na hilo linafanyika ili kuuharibu kabisa msikiti huo na hatimaye kufuta kabisa utambulisho wa kihistoria wa Palestina. Utawala bandia wa Israel daima umekuwa ukilipa kipaumbele suala la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Quds tukufu na kuharibu maeneo matakatifu na ya kihistoria ya mji huo.

Israel hususan katika miongo miwili iliyopita ya mazungumzo na Wapalestina, imejenga majumba ya kamari, mahoteli, vituo vya anasa na maeneo ya ufuska kandokando ya Msikiti wa al Aqsa kwa shabaha ya kuuzingira msikiti huo. Vilevile utawala huo ghasibu unachimba njia za chini ya msikiti huo kwa lengo la kuuharibu.

Katika hali kama hiyo tangu kuasisiwa kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitetea haki za taifa linalokandamizwa la Palestina na kutahadharisha kuhusu matokeo na athari mbaya za kuharibiwa maeneo ya kale ya mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem). Iran pia imetoa wito wa kulindwa Quds na Palestina kama turathi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu katika upeo wa kimataifa.../mh

3349488

captcha