IQNA

Harakati ya Hamas yapinga Mkutano wa Sharm el-Sheikh

22:12 - March 19, 2023
Habari ID: 3476731
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilionyesha upinzani dhidi ya ushiriki wa makundi ya Wapalestina katika mkutano uliopangwa kufanyika huko Sharm El-Sheikh wa Misri unaodaiwa kuwa na lengo la kupunguza hali ya wasiwasi katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Mousa Abu Marzouq, amesema kilichomo katika ajenda za harakati hiyo ni kushadidisha upinzani dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Ameikosoa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa uamuzi wake wa kushiriki katika kikao hicho huku akitoa wito kwa Jumuiya hiyo kuendeleza uratibu na taifa la Palestina badala ya kushirikiana na adui Mzayuni.

Abu Marzouq alionya kuwa utawala wa Israel unapanga mashambulizi mapya dhidi ya Wapalestina wanaokaa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu mwaka 1948 kwa kubomoa nyumba zao.

Vyama na makundi ya mapambano ya Palestina yamemtaka Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuzuia ushiriki wa Wapalestina katika mkutano wa usalama wa Sharm El-Sheikh.

Mkutano wa Sharm El-Sheikh umefanyika nchini Misri leo Jumapili kwa kuhudhuriwa na wajumbe wa kieneo na kimataifa ukiwemo utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na Jordan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina "Safa", vyama vya Democratic Front for the Liberation of Palestine, People's Party na Palestinian Democratic Union (Fedah) vimetoa taarifa ya pamoja vilizitaka Misri na Jordan kufuta mkutano huo na kuacha kuweka mguu katika njia yenye hatari kubwa kwa watu wa Palestina na haki zao.

Makundi hayo yamesema katika taarifa hiyo kwamba maamuzi yatakayopitishwa katika mkutano huo hayatayalazimisha lolote makundi ya Wapalestina.

Taarifa ya makundi ya Palestina inaeleza kuwa mikutano kama hiyo ina sura ya kiusalama inayopingana na  malengo ya wananchi wa Palestina ambayo ni kukomesha uvamizi wa utawala wa Kizayuni, na badala ya kusaidia kuimarisha mshikamano wa ndani kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi wa Wanazi mamboleo, vinawasaidia wavamizi na kuzidisha mgawanyiko na udhaifu.

Haki za wananchi madhulumu wa Palestina zimekuwa zikikandamizwa chini ya buti za utawala ghasibu wa Israel kwa zaidi ya miaka sabini sasa. Katika kipindi chote hicho utawala huo umefanya jinai za kinyama na uhalifu mkubwa zaidi wa kivita na dhidi ya binadamu dhidi ya Wapalestina.

3482852

Kishikizo: palestina hamas misri
captcha