IQNA

Jinai za Israel

Wapigania ukombozi Palestina waapa kulipiza kisasi baada ya Israel kumuua Sheikh Khader Adnan

17:00 - May 02, 2023
Habari ID: 3476946
TEHRAN (IQNA)- Makundi ya kupigania ukombozi (muqawama) Palestina yameapa kuwa yatalipiza kisasi cha damu ya Sheikh Khader Adnan aliyefia shahidi ndani ya jela ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Harakati ya Jihadul-Islami imetangaza kuwa kwa kuuawa mfungwa wa Kipalestina Shahidi Sheikh Khader Adnan, utawala haramu wa Kizayuni ndio unaobeba dhima kamili ya jinai hiyo na utalipa gharama ya unyama huo uliotenda.

Taarifa ya harakati hiyo imesisitiza kwa kusema: "kuuawa shahidi Sheikh Khader Adnan kutakuwa njia ya fikra kwa vizazi vya mashababi shujaa wa siku zijazo; na sisi hatutaiacha njia ya Jihadi na mapambano madamu Palestina inakaliwa kwa mabavu".

Harakati ya Al-Mujahidin imeeleza katika taarifa yake kwamba, adui mzayuni anabeba dhima ya jinai ya kuidhulumu roho ya Khader Adnan na lazima akubali kubeba jukumu la matokeo yote yatakayotokana na jinai hiyo.

Hazem Qassem, msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: "jinai hii ni mauaji ya kinyama ya kimyakimya ambayo yamefanywa na shirika la magereza [la utawala wa Kizayuni] dhidi ya mateka Shahidi Khader Adnan. Wananchi wa Palestina wametuonyesha kuwa jinai hii haiwezi ikaachawa bila kuitolea jibu linalolingana nayo".

Nayo Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina imetangaza kuwa, "uhalifu huo ni operesheni ya mauaji ya mwanamapambano na mmoja wa wafungwa mashuhuri walioanzisha mapambano ya mgomo wa kususia kula. Tunawatolea wito Wapalestina wote waonyeshe hasira zao na kushadidisha muqawama dhidi ya wavamizi na walowezi wao na kufungua medani za mapambano katika Palestina yote".

Nayo Jumuiya ya Palestina ya Wai'd imetangaza kuwa utawala ghasibu wa Israel umetenda jinai iliyovuka kiwango na mipaka yote, hivyo ukae kungojea siku za maafa ndani na nje ya jela zake.

Kufuatia kuuawa shahidi Sheikh Khader Adnan, vijana Wapalestina wametoa wito wa kufanyika migomo katika maeneo yote ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuanzishwa mapambano dhidi ya askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

4137936

captcha