Katika taarifa, mwenyekiti wa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina Zahid Rajan amesema: “Leo Wapalestina wanakabiliana na virusi viwili, kwanza ni kirusi cha utawala wa kibaguzi wa Israel na pili ni kirusi cha COVID-19 na wanapaswa kuagamiza virusi vyote hivyo viwili.” Rajani aidha amesisitiza kuhusu haki ya Wapalestina kurejea katika ardhi zao za jadi na kuondolewa mzingiro wa Ukanda wa Ghaza.
Mwenyekiti wa Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina aidha amesema wanapinga vikali ‘Muamala wa Karne’ na kusema muamala pekee ambao unatakiwa ni ule wa ukombozi wa Palestina.
Halikadhalika ametoa wito kwa wanaharakati wote Palestina kuwa na lengo la pamoja na ukombozi na hivyo wanapaswa kupinga njama zote za kuibua mgawanyiko baina yao.
Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu imeadhimishwa leo Ijumaa ya tarehe 28 Ramadhani, 1441 Hijria inayosaidiana na Mei 22, 2020 Miladia.
Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ndiye aliyeipa siku hiyo ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi Ramadhani jina la Siku ya Kimataifa ya Quds kwa shabaha ya kuakisi dhulma ya kihistoria inayofanywa na Israel, kwa himaya ya madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, dhidi ya watu wanaoendelewa kudhulumiwa na kukandamizwa wa Palestina na ardhi yao takatifu.