IQNA

Waziri wa Masuala ya Kigeni Saudia aunga mkono uhusiano na utawala haramu wa Israel

21:24 - April 02, 2021
Habari ID: 3473778
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Saudi Arabia amedai kuwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuna faida nyingi za kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa eneo la Asia Magharibi.

Faisal bin Farhan Aal-Saud ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Kimarekani  ya CNN alipokuwa akizungumzia uwezekano wa kusainiwa muda si mrefu ujao makubaliano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kifalme wa Saudia na utawala haramu wa Israel na akadaia kuwa, mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida unaendelea, lakini makubaliano hayo yanategemea zaidi kupiga hatua mwenendo wa kufikiwa suluhu na amani baina ya Palestina na Israel.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa Saudia wa kuafiki ndege kutoka Tel Aviv kufanya safari za moja kwa moja kuelekea Makka kwa ajili ya Hija, Bin Farhan amesema, endapo kutakuwapo na upigaji hatua katika suala la Palestina na Israel, raia wa Israel wa dini yoyote ile watakaribishwa kuingia Saudi Arabia.

Katika mahojiano hayo na CNN, waziri wa mambo ya nje wa Saudia alikwepa kutoa jibu kwa suali aliloulizwa kuhusu kuchukuliwa hatua za kisheria mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman kwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi na akasema, Riyadh ina uhusiano imara na serikali ya Marekani na utawala wa Aal Saud ndio mhimili mkuu wa maslahi na vipaumbele vya Washington ndani na nje ya eneo la Asia Magharibi.

Katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliopita wa 2020, nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni na Israel. Inaaminika kuwa Saudia imeonga mkono hatua hizo nyuma ya pazia.

Hatua hiyo ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel imetajwa kuwa ya kihaini na katika fremu ya  kushiriki kwenye mpango wa mapatano wa Kimarekani na Kizayuni, na imeendelea kulaaniwa na kukosolewa vikali na Waislamu na wapenda haki kote duniani.

3962079

Kishikizo: iran saudi arabia
captcha