Sheikh Issa Qassim, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Bahrian ameyasema hayo Alhamisi alipohutubu katika Kongamano la Kimataifa la 'Imam Khomeini na Ulimwengu wa Kisasa"ambao limefanyika katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran. Ameongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kuibua fikra za Kiislamu katika taifa la Iran na kisha katika umma wa Kiislamu duniani na matokeo ya hilo ni kuundwa mrengo wa Mapambano ya Kiislamu.
Akihutubukwa njia ya video katika semina hiyo, Sheikh Issa Qassim amesema leo mhimili wa muqawama unasimama kidete na kwa nguvu zote dhidi ya mradi wa kuanzisha uhusiano na adui Muisraeli. Amesema mradi huo wa kuzishawishi nchi za Kiarabu na Kiislamu zianzishe uhusiano na utawala haramu wa Israel unalenga kuvuruga umma wa Kiislamu. Aidha amesema kusimama kidete huko pia ni kati ya mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain amekumbusha kuwa, mhimili wa muqawama unajumuisha watu ambao ni watiifu kwa umma wa Kiislamu na ambao ni kutoka kaumu, madhehebu na lugha mbali mbali ambapo Iran ya Kiislamu iko katika mstari wa mbele wa harakati zote za mhimili wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.