IQNA

Mufti wa Tanzania: Qur'ani ni kitabu pekee ulimwenguni, kilichoshuka na kupata dhamana ya kuhifadhiwa

18:34 - April 19, 2022
Habari ID: 3475145
TEHRAN (IQNA)- Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zuber, amesema kitabu cha Qur'ani Tukufu ndio kitabu pekee duniani chenye kuhifadhika tofauti na vitabu vingine vyote.

Mufti aliyasema hayo katika fainali ya mashindano ya Qur'ani  Tukufu kitaifa yaliyoandaliwa na Bi. Aisha Sururu Foundation na kufanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar mwishoni mwa wiki.

 “Qur'ani  ni kitabu pekee katika ulimwengu, kilichoshuka na kupata dhamana ya kuhifadhiwa na dhamana ya kukilinda ameichukua mwenyewe Allah. Sisi Waislamu tunakiadhimisha mwezi wa Ramadhan sababu ndio mwanzo wa kushuka kwake” alisema Mufti Zuber.

Aliongeza kuwa Waislamu hawana cha kuwaongoza katika ulimwengu zaidi ya Qur'ani na kwamba ukitafuta kitu nje ya Qur'ani  utakuwa umepotea hivyo akahimiza Waislamu kukitanguliza mbele, kukienzi, kukisoma na kukielimisha kwa wengine.

Aidha Mufti Zuberi alisema kuwa kuna haja ya kuwafuatilia mahafidhi wa Qur'ani  kwa karibu huko walipo, kujua wanaishije, wanafanya nini na kujua idadi yao ili kuwa na takwimu Tanzania ina mahafidhi wangapi, kisha walindwe na watizamwe ili wakatumie kipaji hicho walicho jaaliwa wasije wakaharibika. Mufti Zuberi pia alitaka kuwepo utaratibu wa kuwatambua walimu wanaohifadhisha maneno matukufu ya Qur'ani  ili nao waheshimike zaidi na wathaminiwe kwa kazi hiyo kubwa wanayoifanya.

Katika mashindano hayo ya Qur'ani  kitaifa ya Bi. Aisha Sururu, washindi mbalimbali walipatikana na kupewa zawadi zao. Time Bint Muhammed Mwinyi (5) mlemavu wa macho kutoka mkoani Tanga, alishika nafasi ya kwanza kwa upande wa Juzuu 30.

Bint huyo alivuta hisia za watu kwa hali yake ya kutokuona lakini akiwa mahiri katika kuisoma na kuihifadhi Qur’ani na ndiye aliyeongoza kwa upande wa wanawake.

 Bi. Time ameshinda zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu aina ya Toyo kutoka Aisha Sururu Foundation. Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Ilala Mh. Mussa Azzan Zungu, alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na Bi. Aisha Sururu kumuunga mkono katika Shughuli zake anazozifanya.

Mh. Zungu alisema kuwa mwanadamu mwenye kuisoma Qur'ani  ni bora zaidi ya yule ambaye hana analojua katika Qur'ani , hivyo amewataka Waislamu kuisoma Qur'ani  kwani ndio dira ya maisha ya Muislamu.

Kwa upande mwandaaji wa mashindano hayo Bi. Aisha Sururu, amewashukuru wote waliofanikisha mashindano hayo, wakiwemo majaji kwani wamefanya kazi kubwa na malipo yao watayakuta kwa Mwenyezi Mungu. Aidha aliwashukuru wadhamini wakuu wa mashindano hayo kwa kuwashika mkono na kuwa pamoja nao hadi kufanikiwa kufanyika shughuli hiyo pamoja na wanaharakati wote. Abdallah Athuman Shaweji, aliibuka mshindi wa jumla wa Juzuu 30 katika mashindano hayo.

Ustadh Abdallah alisema kuwa amepokea kwa furaha kubwa ushindi huo, kwani si kwa ujanja wake bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa kumchangua yeye kuwa mshindi wa jumla. Amewataka washiriki wote kutokata tamaa na kuwahimiza kuendelea kuhifadhi na kushiriki mashindano kama hayo na ipo siku wataibuka washindi kwa mapenzi yake Allah (SW).

Gazeti la An-Nuur

captcha