IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Mgahawa wa Ufaransa wamzuia mwanamke Muislamu aliyevaa hijab

20:04 - June 03, 2022
Habari ID: 3475331
TEHRAN (IQNA) - Mgahawa huko Ufaransa haukumruhusu mwanamke Muislamu aliyevaa Hijabu kwa sababu ya vazi lake hilo la Kiislamu.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, tukio hilo lilitokea Jumapili wakati mkazi wa Jiji la Hendaye la Ufaransa, alitaka kumpeleka mama yake kwenye mgahawa kwa chakula cha jioni cha Siku ya Mama, na alikuwa ameweka nafasi hiyo  wiki moja mapema.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, wakati mama na mwanae wa kiume walipofika kwenye mlango wa mgahawa, mwanamke ambaye anamiliki biashara hiyo alisema hatawaruhusu wateja hao wawili kwenye mgahawa kwa sababu mama yake amevaa "mtandio kichwani ambao ni wa Zama za Giza."

Mmiliki wa mgahawa, ambaye anaaminika kuwa Mkristo kwa sababu alikuwa amevaa nembo ya kidini - msalaba shingano - alidai kwamba "mtandio ni chombo kinachotumika kuwakandamiza wanawake" na kwa msingi huo alikataa kumruhusu mwamamke huyo Muislamu kuingia katika mgahawa.

Baada ya kuzuiwa, wawili hao walifika katika  kituo cha polisi na kutoa malalamiko ya kubaguliwa kinyume cha sheria..

Tukio hilo limelaaniwa vikali katika mitandao ya kijamii na kutajwa kuwa ni ubaguzi na chuki ya wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Kufuatia kutekelezwa  sheria zinazolenga Waislamu huko Ufaransa, hujuma dhidi ya Waislamu, hasa wanawake wanaovaa Hijabu zimeongezeka sana.

Halikadhalika vituo vya Kiislamu vimekuwa vikishambuliwa mara kwa mara na watu wenye chuki ambao wamepata msukumo kutoka sera dhidi ya Uislamu za serikali.

Hivi karibuni, uamuzi wa manispaa ya Grenoble wanawake Waislamu kuvaa mavazi maalumu ya kuogelea yanayowasitiri ulisitishwa na korti kufuatia  maagizo ya Waziri wa Mambo ya ndani Gerald Darmanin.

Mwaka uliopita,  Bunge la Kitaifa la Ufaransa liliidhinisha sheria ya 'Thamani za Jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Jumuiya ya Waislamu Ufaransa (CFCM) imepinga vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa yenye kuwawekea Waislamu vizingiti katika maisha yao yote.

Sheria hiyo inaipa serikali haki ya kuingilia mambo ya misikiti kama vile hotuba na kupeleleleza kamati zinazosimamia misikiti na pia kudhibiti matumizi ya pesa za misikiti na asasi za Waislamu.

3479153

captcha