IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu Ufaransa

Mpango wa Ufaransa wa kuwatimua viongozi wa jamii za Waislamu

18:58 - September 07, 2022
Habari ID: 3475748
TEHRAN (IQNA)- Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu katika mataifa ya Ulaya hususan Ufaransa ungali unaendelea huku kukiwa na mpango wa kuwatimua Maimamu na viongozi wengine wa jamii ya Waislamu katika nchi hiyo.

Katika fremu hiyo, Baraza la Utawala la Ufaransa, limeidhinisha hukumu ya kufukuzwa nchini humo Hassan Iquioussen Imam wa Swala ya Jamaa mwenye asili ya Morocco kwa tuhuma za kueneza chuki dhidi ya Mayahudi. Pamoja na hayo, hukumu hiyo imekabiliwa na malalamiko na upinzani wa akthari ya wananchi wa Ufaransa huku mamia ya watu wakikusanyika katika mji mkuu Paris kulalamikia uamuzi huo.

Waandamanaji wamelaani kile walichokitaja kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ya viongozi wa Ufaransa. Zaidi ya misikiti 31 kaskazini mwa Ufaransa imetoa taarifa ikitangaza kumuunga mkono Sheikh Hassan Iquioussen na kumtaja kuwa mhanga wa makosa ya wazi ya tathmini ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo ya bara Ulaya.

Pamoja na hayo, Gerald Darmanin, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ufaransa amesema kuwa, kuidhinishwa hukumu ya kutimuliwa nchini humo kiongozi huyo wa kidini ni ushindi kwa Jamhuri ya Ufaransa.

Sheikh Hassan Iquioussen mhadhiri wa Kifaransa ni mwasisi wa Jumuiya ya Vijana Waislamu nchini Ufaransa. Mhadhiri huyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Mayahudi na thamani za kisekulari nchini Ufaransa. Hotuba zake zimeifanya serikali ya Ufaransa ichukue uamuzi wa pupa wa kumfukuza nchini humo.

Lucie Simon, wakili wa Sheikh Hassan Iquioussen amesema, katika miezi ijayo ataendeleza mapambano ya kutaka kutambuliwa ukiukaji wa uhuru wa kujieleza wa mteja wake na ukiukaji uliofanyika wa kumtimua nchini humo.

Hii si hatua ya kwanza kwa serikali ya ufaransa dhidi ya Waislamu. Katika miaka ya hivi karibuni, chuki dhidi ya Uislamu zimekuwa moja ya sera za serikali za Ulaya na makundi yenye kufurutu ada.

Makundi hayo yakitumia visingizio mbalimbali yamekuwa yakiushinikiza Uislamu na Waislamu sambamba kuwaandama kwa vitendo vya chuki, uadui na maudhi. Hii ni katika hakli ambayo, viongozi wa Ulaya wamekuwa wakipigia upatu suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni sambamba na uhuru wa kisiasa katika bara hilo.

Hivi karibuni duru zilidokeza kuwa kuna orodha ya maimamu watakaotimuliwa na inatayarishwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, na baadhi ya vyama vya kisiasa Ufaransa vinataka kushirikishwa katika kuitayarisha.

Orodha hii inajumuisha majina 15 ya maimamu wa misikiti ya nchi hiyo wanaotuhumiwa kwa kueneza chuki, ubaguzi na ukiukaji wa maadili ya jamhuri, na juhudi zinafanywa kuwafukuza nchini.

Vyanzo vilivyo karibu na Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha misimamo mikali ya mrengo wa kulia, ambaye alishindwa na  Emmanuel Macron katika uchaguzi wa rais wa Ufaransa, amesema kwamba maimamu hao wa misikiti wanatoka nchi za Kaskazini mwa Afrika na nchi kama vile Morocco, Algeria na Tunisia.

 

4083522/

captcha