IQNA

Kadhia ya Palestina

Marekani yatumia kura ya turufu kupinga uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa

17:41 - April 19, 2024
Habari ID: 3478702
IQNA-Marekani, ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala haramu wa Israel, imeendeleza sera yake ya kudhoofisha kupatikana haki za Wapalestina kwa kutumia vibaya haki yake ya kura ya turufu na kupinga azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Marekani, ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, imeendeleza sera yake ya kudhoofisha kupatikana haki za Wapalestina kwa kutumia vibaya haki yake ya kura ya turufu na kukwamisha azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Ofisi ya kiongozi wa Mamlaka ya Palestina (PA) Mahmoud Abbas imeita kura ya turufu ya Marekani kuwa ni "uchokozi wa wazi... ambao unasukuma eneo hilo zaidi kwenye mgogoro."

"Ukweli kwamba azimio hili halijapitishwa hautavunja nia yetu, na hautashinda azma yetu," balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, alisema kufuatia kura hiyo.

“Hatutakoma katika juhudi zetu. Taifa huru la Palestina haliepukiki. Ni uhakika," alisema.

Amar Bendjama, balozi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa amesema uungaji mkono mkubwa wa Palestina "unatuma ujumbe wazi" kwamba Palestina ni nchi mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa na mchakato wa uanachaam wa Palestina utarudi tena kwa nguvu zaidi.

Harakati ya Mapamabano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas,  pia imekashifu hatua hiyo ya Marekani. "Hamas inalaani kura ya turufu ya Marekani katika Baraza la Usalama dhidi ya rasimu ya azimio la kuipa Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa," ilisema katika taarifa.

Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia ametoa mjibizo kwa hatua ya Marekani ya kutumia kura yake ya turufu kupinga uwanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, lengo la Marekani ni kuvunja irada ya Wapalestina na kuwafukuza katika ardhi yao.

Kwa sasa, Palestina mtazamaji wa kudumu katika Umoja wa Mataifa. Mnamo mwaka 2011, taifa hilo madhulumu liliomba uanachama wa kudumu katika umoja huo.

Mwezi Aprili, Palestina ilituma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiomba lifikirie upya ombi lake la kujiunga na Umoja wa Mataifa kwa sura ya mwanachama wa kudumu.

Kura hiyo ya turufu inajiri wakati uvamizi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza uliozingirwa umeua takriban watu 34,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

3487990

Kishikizo: marekani palestina
captcha