IQNA

UNRWA: Wakimbizi Wapalestina wanaishi katika hali mbaya sana

10:45 - March 22, 2015
Habari ID: 3023920
Wakimbizi Wapalestina walio katika nchi mbali mbali duniani wanakabiliwa na matatizo makubwa sana. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetoa onyo kuhusu hali mbaya sana ya wakimbizi Wapalestina.

Msemaji wa UNRWA Christopher Gunness ametoa taarifa na kusema kuwa Wapalestina 59 walipoteza maisha tarehe tano mwezi huu wa Machi wakati boti yao ilipokumbwa na dhoruba katika Bahari ya Mediterranea  karibu na kisiwa cha Sicily cha pwani ya Italia. Amesema wakimbizi wao walikuwa wametoka Syria, Lebanon na Ukanda wa Ghaza na jambo hilo ni ishara kuwa wanakumbwa na hali mbaya ya kimaisha walikotoka. Wapalestina walioko katika Ukanda wa Ghaza wanakumbana na jinai zisizo na kikomo za utawala haramu wa Israel. Wakimbizi Wapalestina walioko Syria nao wamejipata kati kati ya mapigano makali nchini humo huku waliokimbilia nchi jirani ya Lebanon wakikumbwa na hali mbaya ya kimaisha kambini. Hivyo  wengi wanakuwa hawana budi ili kutafuta kimbilio maeneo mengine duniani. Hakuna shaka kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopiota dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la wakimbizi.
Watu wa nchi kama vile Syria, Iraq, Libya, Sudan, Nigeria, Somalia na hata Ukraine wamelazimika kuzikimbia nchi zao kufuatia kuongezeka mapigano na ukosefu mkubwa wa usalama. Baadhi wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi zao na kukimbilia maeneo hatari kama juu ya milima kama ilivyshudiwa nchini Iraq.  Jambo la kusikitisha idadi kubwa ya wakimbizi wanakumbwa na hali mbaya sana kutokana na kuwa  jamii ya kimataifa haijachukua hatua za kutosha kuwasaidia.  Kati ya jamii muhimu zaidi ya wakimbizi duniani ni ile ya Wapalestina.  Kwa uchache kuna Wapalestina takribani milioni tano waliotapakaa katika nchi mbali mbali kama wakimbizi. Baadhi ya Wapalestina wameshapewa uraia na nchi zilizowapokea. Idadi kubwa ya wakimbizi hao milioni tano wanakumbwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa chakula na maji safi, suhula duni za afya , ukosefu wa ajira, ubaguzi, ukiukwaji wa haki za binadamu n.k.
Halikadhalika idadi kubwa ya wakimbizi Wapalestina wanaishi nchini Syria nchi ambayo inakabiliwa na vita vya ndani vilivyoibuliwa na magaidi wa kitakakfiri. Aidha Wapalestina wanaoishi Lebanon pia wanakumbwa na matatizo kutokana na athari mbaya za vita vya Syria nchini humo. Idadi kubwa ya Wasyria wamekimbilia Lebanon na hivyo kuifanya nchi hiyo ishindwe kukabiliana na idadi kubwa ya wakimbizi.
Hivi sasa Wapalestina wanaokabiliwa na matatzio katika nchi hizo wanatumia kila njia kujaribu kukimbilia nchi za mbali zaidi. Baadhi ya nchi hizo wanazotumia zimejaa hatari na wengi hupoteza maisha wakijaribu kukimbia. Ni kwa msingi huo ndio tumeshuhudia makumi ya Wapalestina wakipoteza maisha katika Bahari ya Mediterranea wakijaribu kufika Ulaya. Jamii ya kimataifa na nchi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu zinapaswa kuchukua hatua kuwanusuru Wapalestina ambao badala ya kupata salama baada ya kukimbia jinai za utawala haramu wa Israel, wangali wanakumbwa na masaibu walikokimbilia.
Hivi karibuni pia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilisema hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ni mbaya kupindukia na limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel kuondoa mzingiro wake wa kidhulma na kikatili dhidi ya eneo hilo.
Mkurugenzi wa UNRWA, Robert Tuner alisema umasikini, ukosefu wa ajira na kuporomoka uchumi kulikosababishwa na mzingiro wa Wazayuni katika Ukanda wa Gaza kumesababisha hali ya eneo hilo kuwa ya kusikitisha. Tuner alisema iwapo Israel haitashinikizwa kuondoa mzingiro wa Gaza, hali ya mambo itazidi kuwa mbaya. Mkuu wa UNRWA ameashiria vita vya mwaka uliopita vya Israel katika Ukanda wa Gaza na kusema vita hivyo mbali na kuharibu makazi mengi ya Wapalestina vimezidisha mateso na madhila kwa Wapalestina hususan wanawake na watoto.
Vita vya siku 50 vya Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza mwaka uliopita vilisababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 2000 wengi wao wakiwa watoto wadogo na wanawake.../mh

3020900

captcha