IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu / 22

Mapendekezo ya Kiuchumi ya Shuaib, Mtume wa Mwenyezi Mungu

20:37 - December 21, 2022
Habari ID: 3476282
TEHRAN (IQNA) – Shuaib –Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake- (AS) alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na dhuria wa Ibrahim (AS). Shuaib (AS) ni nabii wa tatu wa Kiarabu ambaye jina lake limetajwa katika Qur'ani Tukufu.

Baba yake alikuwa Madin mtoto wa Ibrahim (AS) na mama yake alikuwa binti wa Nabii Lut (AS). Wengine wanaamini Madin alikuwa babu yake na jina la baba yake lilikuwa Nuaib. Pia kuna maoni tofauti kuhusu kama Shuaib alikuwa baba mkwe wa Musa (AS) ambaye jina lake limetajwa katika Agano la Kale kama Yethro.

Aidha Agano la Kale halijataja kisa cha Shuaib na watu wake bali kilichosemwa tu ni kwamba baada ya Musa (AS) kuondoka Misri na kwenda Madyan, alikutana na mtu aitwaye Reuel, ambaye alikuwa mamlaka ya kidini katika mji huo na wengine wanaamini kuwa alikuwa Shuaib.

Katika zaidi ya aya 40 katika Sura Al-Araf, Hud, Ash-Shu’ara, Al-Ankabut na Al-Qasas, Qur'ani Tukufu inamtaja Shuaib, ingawa jina lake limetajwa moja kwa moja mara 11. Nyingi ya aya hizo zinahusu mada kama vile usimamizi, haki za jamii, maadili, ukuzaji wa utamaduni wa kuamini Mungu mmoja, na mageuzi ya kiuchumi. Aya pia zinazungumzia wale waliokataa wito wa Shuaib na adhabu waliyoipata.

Shuaib alikuwa nabii baada ya Yusuf (AS), mwana wa Yakub (AS), na kabla ya Musa (AS). Anaaminika kuwa nabii wa tatu wa Kiarabu ambaye kisa chake kimetajwa katika Qur'ani Tukufu.

Madyan, au Madyan Shuaib, ni mji katika Ghuba ya Aqaba huko Bara Arabi. Shuaib aliishi kwanza katika mji huu. Aliwaita watu wa mji huo kumwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuepuka kufanya maovu, lakini waliukataa mwito wake na wakamfukuza Shuaib na wafuasi wake katika mji huo.

Shuaib akawalaani na Mwenyezi Mungu akaleta tetemeko la ardhi kuwaadhibu. Mji uliharibiwa na watu wake waliuawa kwa tetemeko la ardhi.

Kisha Shuaib akaenda kwa watu wa Ikka, mji ulio karibu na Madyan ambao sasa unajulikana kama Tabuk. Qur'ani Tukufu inasema kwamba watu wa Ikka pia walikataa mwito wa Shuaib na wakasisitiza juu ya ukafiri wao. Kwa hivyo pia waliuawa katika adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Katika aya ya 85 ya Surah Al-Araf, Mwenyezi Mungu anasema kwamba watu wa Madyan hawakufuata kanuni za biashara na maingiliano ya kiuchumi. Shuaib alijaribu kurekebisha mwenendo wao wa kiuchumi lakini hawakufuata ushauri wake: “ Na kwa watu wa Madyan tulimtuma ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwisha kufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.”

captcha