IQNA

Waislamu Kanada

Kanada yamteua Mwakilishi Maalum Kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

18:22 - January 27, 2023
Habari ID: 3476474
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Kanada (Canada) imemteua Amira Elghawaby kama mwakilishi wa kwanza maalum wa nchi hiyo katika kupambana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Elghawaby anaongoza kitengo cha mawasiliano cha kimkakati kwa Shirika la Mahusiano ya Kirangi Kanada na alikuwa mmoja wa wajumbe wa bodi waanzilishi wa Mtandao wa Kupambana na Chuki wa Kanada. Pia ni mwanachama katika Kikundi cha Ushauri wa Uwazi wa Usalama wa Kitaifa, ambacho humshauri naibu waziri wa usalama wa umma kuhusu sera ya usalama wa kitaifa.

"Chuki dhidi ya Uislamu na tabia nyingine za chuki dhidi ya wageni, ikiwa ni pamoja na chuki dhidi ya Wayahudi, ubaguzi wa rangi dhidi ya wenye asili ya Afrika, chuki dhidi ya jamii za wakazi asili wa Kanada na ubaguzi wa rangi dhidi ya Waasia ni matatizo yanayoendelea kuwepo katika jamii ya Kanada, licha ya itikadi za maelewano baina ya tamaduni  ambazo mimi na wengine wengi tulikua tukiiamini," Elghawaby alisema huko Toronto siku ya Alhamisi.

Alisema anatumai jukumu lake jipya – ambalo ni la kwanza la aina yake ulimwenguni linalosimamiwa na serikali - litaboresha uelewa wa Kanada wa "utambulisho n utamaduni za Waislamu," huku pia likipinga "ubaguzi wa rangi na upotoshaji" unaoikabili jamii hiyo.

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Kanada (NCCM) kwa mara ya kwanza liliitaka serikali ya nchi hiyo kuunda nafasi hiyo baada ya watu wanne wa familia moja ya Kiislamu kuuawa mwaka 2021 wakati dereva wa lori alipowagonga kwa makusudi walipokuwa wakitoka kwa matembezi ya jioni  mji wa London jimboni Ontario. Fayez Afzaal mwenye umri wa miaka tisa ndiye pekee aliyenusurika katika shambulio hilo, ambalo polisi wa London walisema lilichochewa na chuki dhidi ya imani ya familia hiyo.

Ombi hilo liliibuliwa na maafisa wa serikali katika mkutano wa kilele wa kitaifa ulioitishwa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu mwezi Julai 2021. Wakati huo, NCCM ilitaka kuona mwakilishi wa aina hiyo akipewa “mamlaka ya kamishna wa kuchunguza masuala tofauti yanayohusu chuki dhidi ya Uislamu nchini Kanada, na kuwa na uwezo wa kukagua katika sekta zote za serikali ya shirikisho kuhusiana na wasiwasi kadhia ya chuki dhidi ya Uislamu.

Serikali ya Kanada ilitangaza kuwa imeanza kumtafuta mwakilishi huyo maalum Juni mwaka jana, baada ya kutoa dola milioni 5.6 kwa miaka mitano katika bajeti ya serikali ya 2022 kufadhili nafasi hiyo.

Waziri wa Anuwai na Ushirikishwaji Ahmed Hussen alisema Alhamisi kwamba Elghawaby atafanya kazi kwa karibu na maafisa wa serikali ili kupambana na chuki dhidi ya Waislamu nchini Canada, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ili kulinda uhuru wa dini na kuboresha sera za umma.

3482228

captcha