IQNA

Kadhia ya Palestina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Gaza imeamsha dhamiri ya mwanadamu, nchi za Kiislamu ziisusie Israel

15:54 - November 01, 2023
Habari ID: 3477822
TEHRAN (IQNA)- Katika kueleza mafanikio ya subira na kusimama kidete Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Watu wa Ghaza wameamsha dhamiri ya mwanadamu kwa subira yao.

Akizungumza katika kikao na maelfu ya wanafunzi na wanachuo wa Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyataja maafa  yaliyosababishwa na Wazayuni na Wamarekani huko Ghaza kuwa ni makubwa sana katika historia na kusema: "Nyoyo zetu zinavuja damu kwa ajili ya mateso wanayokumbana nayo wananchi wa Palestina hususan Ghaza, lakini tukitazama kwa kina eneo hilo, inatubanikia wazi kuwa mshindi katika medani hii ni watu wa Ghaza na Palestina ambao wameweza kufanya mambo makubwa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuondolewa pazia bandia la haki za binadamu ambalo lilikuwa limefunika nyuso za Wamagharibi na baada ya hapo kufedheheka kwao  ni miongoni mwa matokeo ya subira na muqawama au mapambano ya watu wa Ghaza na kuongeza kuwa: "Watu wa Ghaza wameamsha dhamiri ya mwanadamu kwa uvumilivu wao; Unaona leo, hata katika mitaa ya Marekani na nchi za Magharibi, umati mkubwa wa watu wanatoa nara dhidi ya Israeli na katika maeneo mengi pia dhidi ya Marekani."
Ayatullah Khamenei akiashiria mapigo ya kufedhehesha ambayo subira na misimamo ya watu wa Ghaza imetoa kwa itibari na haiba ya utawala huo ghasibu na waungaji mkono wake wenye kiburi amesema: “Iwapo hakutakuwa na msaada wa kina kutoka kwa Marekani, basi utawala wa Kizayuni utapooza ndani ya siku chache."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ametaja mauaji ya watoto elfu nne ndani ya wiki tatu kuwa ni jinai isiyo na kifani katika historia ambayo imetendwa na Israel, na kusisitiza kuhusu kuwa macho Umma wa Kiislamu kuhusiana na matukio ya Ghaza, eneo ambalo kwa hakika ni uwanja wa mapambano kati ya "haki na batili" na "imani na kiburi". Ameendelea kusema kuwa nguvu ya madola yenye kiburi na ya kiistikbari inakuja na mabomu, mashinikizo ya kijeshi, maafa na uhalifu, lakini nguvu ya imani itashinda haya yote kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya ulazima wa kuleta pamoja ulimwengu wa Kiislamu na haja ya serikali za Kiisalmu kusistiza kuhusu kusimamishwa mara moja jinai na udondoshaji wa mabomu huko Ghaza. Halikadhalika amezitaka serikali za Kiislamu zizuie usafirishaji wa mafuta na chakula kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuususia utawala huo kiuchumi. Pia ametaka nchi za Kiislamu kuulani jinai za kinyama za utawala ghasibu wa Israel katika majukwaa yote ya kimataifa bila kigugumizi  au undumakuwili.

Akiashiria namna walivyofedheheka wanaoeneza uongo duniani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema kuwataja wapiganaji wa Palestina kuwa eti ni magaidi ni ishara ya kukosa aibu wanasiasa na vyombo vya habari vya Magharibi. Ayatullah Khamenei ameendelea kwa kuhoji hivi: Je, yeyote anayeitetea nyumba na nchi yake ni gaidi? Je, Wafaransa waliopigana na Wajerumani huko Paris katika Vita vya Pili vya Dunia walikuwa magaidi? Inakuwaje wao ni wapiganaji na ni fahari kwa Ufaransa, lakini vijana wa Jihad Islami na Hamas ni magaidi?

3485839

Habari zinazohusiana
captcha