IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Historia haitasahau jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuua wanawake na watoto

21:32 - January 09, 2024
Habari ID: 3478174
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, njama kubwa za maadui ni kuwatoa uwanjani wananchi wa Iran na kwamba Ukanda wa Gaza hivi sasa ni mfano wa wazi na wa kivitendo wa nguvu kubwa za wananchi huku akisisitiza kuwa historia haitasahau jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wanawake na watoto Wapalestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumanne jijini Tehran wakati alipoonana na maelfu ya wananchi wa Qum katika maadhimisho ya mapambano ya kihistoria ya wananchi wa Iran ya Dei 19, 1356 (Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 9 Januari 1978 Milaadia).

Utawala kibaraka wa Shah ulifanya mauaji makubwa na ya kutisha dhidi ya wananchi wa Qum wakati wa mapambano hayo lakini mauaji hayo yakawa ndio mwanzo wa kupata nguvu harakati kubwa ya wananchi Waislamu wa Iran iliyoishia kwenye kupinduliwa utawala wa kiimla wa Shah na kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Februari 11, 1979 humu nchini.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Ukanda wa Gaza hivi sasa ni dhihirisho la wazi la nguvu kubwa za wananchi na kusisitiza kuwa, kundi dogo tu la wananchi tena katika sehemu ndogo tu ya ardhi limewakwamisha na kuwafelisha Marekani na utawala wa Kizayuni licha ya majigambo yao makubwa. Kundi hilo la wananchi wa Gaza limeonesha nguvu zao za subira na kusimama imara mbele ya adui. 

Amesema jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni za kuua watoto wadogo na wanawake huko Gaza haziwezi kusahaulika katika historia na kusisitiza kuwa, hata baada ya kuangamizwa na kufutwa utawala wa Kizayuni kwenye uso wa dunia, kumbukumbu ya jinai za utawala huo itabakia na kati jinai hizo hazitosauliwa.

Amesema, historia itaendelea kuandika kwamba katika kipindi cha wiki chache tu, kundi fulani kwenye eneo hili lilifanya mauaji ya maelfu ya watoto, lakini subira,  mapambano (muqawama) na kusimama kidete wananchi wa Palestina kulililazimisha kundi hilo kukimbia.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aidha amesema kuwa, kuwatishia watu kuhusu nguvu za Marekani na utawala wa Kizayuni ni hila nyingine ya kujaribu kuwatoa uwanjani watu lakini amesema:  Lau kama kazi ya taifa la Iran ingelikuwa ni kugopa nguvu za dola fulani, hivi sasa isingelikuwepo tena Jamhuri ya Kiislamu kama ambavyo pia madola mengi makubwa yaliyokuwa yanajigamba kuwa na nguvu kubwa na kudhibiti kila kitu kwenye eneo hili, hivi sasa yanaliogopa taifa la Iran.

 

 

3486750

Habari zinazohusiana
captcha