IQNA

Jinai za Israel

ICJ yautaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mauaji ya kimbari Gaza

21:11 - January 26, 2024
Habari ID: 3478258
IQNA-Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ hii leo imeamua kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel lazima uchukue hatua zote za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari katika mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina huko, Gaza.

Uamuzi unaofuatia shauri lililowasilishwa na Afrika Kusini la kutaka Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ichukue hatua za awali kwa mujibu wa Mkataba wa kimataifa wa kuepusha mauaji ya kimbari wa mwaka 1948.

Afrika Kusini katika shauri lake iliyowasilisha tarehe 29 mwezi Desemba mwaka jana wa 2023, ilisema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unakiuka wajibu wake wa kuzingatia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia mauaji ya Kimbari kuhusiana na Wapalestina huko Ukanda wa Gaza na hivyo kutaka ICJ ichukue hatua za awali kuepusha kinachoendelea.

Hatua ni pamoja na Israel isitishe mara moja operesheni zake za kijeshi ndani na dhidi ya Gaza, ichukue hatua za kimsingi kuepusha mauaji ya kimbari na pia ichukue hatua zote ndani ya uwezo wake kufuta amri zinazohusiana na mashambulizi ikiwemo za kuzuia au kufukuza na kufurusha watu kutoka makazi yao, halikdhalika watu kunyimwa fursa ya kupata chakula cha kutosha na maji.  

Hukumu ya ICJ yenye kurasa 29 iliyosomwa na Jaji Joan E. Donoghue  inasema masharti yote ya kuwezesha kuchukua hatua za dharura yako wakati uamuzi wake wa mwisho ukisubiri wa kutangaza hatua za kulinda haki zilizowasilishwa na Afrika Kusini. 

Mahakama imesema kwa mazingira ya kesi husika, hatua zitakazochukuliwa si lazima zifanane na zile zilizoombwa na Afrika Kusini.

Kwa hivyo basi Israeli inapaswa, kwa mujibu wa Mkataba wa kuzuia mauaji ya kimbari ambayo utawala huo ni mwanachama, itumie uwezo wake wote izuie vitendo vyote kwa mujibu wa ibara ya pili ya mkataba huo ikiwemo mauaji dhidi yaWapalestina.

Aidha ICJ imeutaka utawala wa Israel uzuie mauaji yoyote ya Wapalestina Ukanda wa Gaza na ichukue hatua zote kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu eneo hilo.

Mahakama imetaka Israel iwasilishe ripoti ya utekelezaji wa uamuzi huu wa Mahakama ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe ya leo ya hukumu, ripoti ambayo itawasilishwa pia kwa Afrika Kusini ili nayo iweze kutoa maoni yake kuhusu utekelezaji. 

Suala hili lilikuwa miongoni mwa maombi ya Afrika Kusini ya kwamba ripoti ya utekelezaji iwasilishwe.

Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha ICJ, uamuzi unaotolewa na Mahakama hii huwa haukatiwi rufani.

Afrika Kusini imekuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Wapalestina na imechukua hatua  kuiwajibisha Israel kwa vitendo vyake huko Gaza. Nchi hiyo ya Kiafrika, ambayo imepitia miaka mingi ya utawala wa kibaguzi, imesifiwa na wanaharakati kuwa kinara wa dhamiri ya kimataifa na sauti ya wanyonge.

Takriban Wapalestina 26,083, karibu asilimia 70 kati yao wanawake, watoto wadogo na vijana, wameuawa katika Ukanda wa Gaza katika mashambulizi ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel kwa himaya ya Marekani dhidi ya eneo hilo tangu Oktoba 7.

3486959/

captcha