IQNA

Kadhia ya Palestina

Raia wa Afrika wanaoshiriki katika vita vya Israel dhidi ya Gaza kukamatwa wakirejea nyumbani

6:28 - March 16, 2024
Habari ID: 3478520
IQNA-Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini amesema kuwa, raia yeyote wa nchi hiyo atakayeusaidia utawala wa Kizayuni katika vita vya Ukanda wa Gaza atatiwa mbaroni punde tu atakaporejea Afrika Kusini.

Hayo yameelezwa na Naledi Pandor Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini katika hafla ya mshikamano na Wapalestina iliyofanyika mbele ya viongozi wa chama tawala cha Congress ya Taifa ya nchi hiyo na kuongeza kuwa, raia wa nchi hiyo wanaopigana katika jeshi la Kizayuni au pamoja nao katika Ukanda wa Gaza watatiwa mbaroni baada ya kurejea nchini Afrika Kusini.

Waziri huyo ambaye anafahamika kwa misimamo yake thabiti ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina amewatolea mwito watu wa nchi yake kukusanyika na kuandamana mbele ya balozi za nchi zinazoiunga mkono Israel.

Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele kupinga na kulaani vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7. Mwaka jana, nchi hiyo ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ huko The Hague, Uholanzi ikiituhumu Israel kwa mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.

Tarehe 29 Disemba mwaka 2023, Afrika Kusini iliwasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ huko The Hague Uholanzi ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kwa kukiuka Makubaliano ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1948 wakati wa operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza. 

Israel ilianzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, wapalestina wasiopungua 31,000 wameuawa na zaidi ya 73,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel. Takriban asilimia 72 ya waathiriwa ni watoto na wanawake.

Zaidi ya miezi mitano ya mashambulizi ya kikatili ya Israel pia yamesababisha njaa kali miongoni mwa Wagaza huku takribani asilimia 60 ya miundomsingi ya eneo hilo ikiwa imeharibiwa.

3487570

Habari zinazohusiana
captcha