IQNA

Waislamu India

Wahindu wenye chuki na Uislamu wamuua Imamu na kuuchoma moto msikiti nchini India

17:26 - August 01, 2023
Habari ID: 3477368
TEHRAN (IQNA)- Naibu Imamu wa Sala ya jamaa ameuawa baada ya kundi la Wahindu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kuufyatulia risasi na kuuchoma moto msikiti katika kitongoji cha mji mkuu wa India, New Delhi, saa chache baada ya ghasia mbaya za kijamii zilizozuka katika wilaya jirani.

Polisi wamemtaja Imamu huyo aliyeuawa kuwa ni Maulana Saad mwenye umri wa miaka 19, anayesalisha msikiti wa Anjuman Jama ulioko katika sekta ya 57 ya Gurugram, jiji la watu milioni moja na laki mbili linalojulikana kwa minara yake ya kumeta na ofisi za mashirika ya kimataifa.

Watu wengine watatu walikuwepo eneo la hujuma hiyo, ambapo mmoja alijeruhiwa na wawili walinusurika na hujuma hiyo.

Msikiti huo umeshambuliwa na umati wa Wahindu wenye chuki na Waislamu mapema leo, siku moja baada ya ghasia zilizozuka katika wilaya jirani ya Nuh kaskazini mwa jimbo la Haryana.

Naibu Kamishna wa Polisi Nitish Agarwal, amesema, kundi la wahuni wapatao 50 hadi 60 waliamua kufyatua risasi na kuanzisha uchomaji moto katika mji wa Anjum mapema leo, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kumjeruhi mwingine.

Hayo yanajiri wakati kundi la Wahindu la mrengo mkali wa kulia lenye mfungamano na chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) limekuwa likiendesha kampeni ya kupiga marufuku Sala ya Ijumaa katika mji wa Gurugram, ulioko kwenye jimbo la Haryana. Msikiti wa Anjuman ni miongoni mwa maeneo machache yaliyokubaliwa rasmi kutumika kwa ajili ya Sala hiyo.

Tukio hilo limefuatia mapigano makali kati ya jamii za Wahindu na Waislamu huko Nuh, ambako vyombo vya dola vimetangaza marufuku ya kutotoka nje.

Takriban watu wanne, wakiwemo maafisa wawili wa polisi waliuawa katika mapigano hayo yaliyozuka katika wilaya hiyo ya Nuh.

Ghasia na mapigano hayo yalizuka wakati maandamano ya kidini ya Wahindu yalipopitia eneo hilo lenye Waislamu wengi.

3484598

Habari zinazohusiana
Kishikizo: india waislamu
captcha