IQNA

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Mwanazuoni wa Lebanon: Umoja ni msingi muhimu wa kulinda Uislamu

9:26 - October 11, 2022
Habari ID: 3475911
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni mwandamizi wa Lebanon ameutaja umoja kati ya Waislamu kama msingi imara zaidi wa kulinda Uislamu kutokana na vitisho vilivyopo.

Sheikh Ghazi Hanina, Mkuu wa Majlisi ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon ameyasema hayo alipokuwa akihutubia Kongamano la 36 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu kwa njia ya intaneti jana Jumatatu.

“Baada ya kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, umoja wa Kiislamu ndiyo silaha yenye nguvu zaidi, kwa sababu umoja huu unajenga usalama na kulinda dini ya Kiislamu, mali ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu na ulimwengu wa Kiarabu, pamoja na suala la Palestina. Kama mnavyofahamu, suala la Palestina ni moja ya dhihirisho la umoja wa Kiislamu kati ya Shia na Sunni” alisema.

 "Wale wanaotaka kuusambaratisha Ummah wa Kiislamu na hawafurahii kuona Ummah huu ukiendelea kwa namna yoyote ile ndio wanaoinama mbele ya adui Mzayuni na kuingia katika mchakato wa kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni," aliongeza.

Akizungumzia muqawama au mapambano ya  wananchi wa Palestina amesema: "Leo ni vijana wa Kipalestina, wanawake wa Kipalestina na wanaume wa Kipalestina ambao wanasimama na kukabiliana na adui dhalimu wa Kizayuni kwa kutegemea chaguo la Muqawama."

 "Kuelezea kanuni za Uislamu safi ambazo Mtukufu Mtume (SAW) na familia yake safi walituletea ni mojawapo ya njia zenye ufanisi zaidi za kukabiliana na ugaidi wa wakufurishaji," aliongeza.

Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu imeaandaa toleo la 36 la Kongamano la Umoja wa Kiislamu ambapo ushiriki kupitia vikao vya itaneti au webinar ukiwa umeanza Oktoba 9 huku kongamano hilo likitazamiwa kufunguliwa rasmi 12 Oktoba na kuendelea hadi Ijumaa kwa kushirikisha wanazuoni wengi wa Kiislamu kutoka nchi 60.

Jumuiya hiyo imekuwa ikiandaa kongamano la kimataifa la Umoja wa Kiislamu kila mwaka kwa muda wa miaka 35 sasa.

Kongamano hilo kwa kawaida hufanyika Tehran, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Tuko katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama siku za Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

568502

captcha