IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

OIC yaitisha mkutano wa dharura baada ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi

13:32 - July 01, 2023
Habari ID: 3477220
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetangaza mkutano wa dharura kufuatia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu hivi karibuni katika mji mkuu wa Stockholm wa Uswidi.

Shirika la Habari la Saudia (SPA) liliripoti siku ya Ijumaa kwamba Kamati ya Utendaji ya jumuiya hiyo ya kiserikali itakutana wiki ijayo kwa mwaliko wa Ufalme wa Saudi Arabia kushughulikia suala hilo.

Kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, ambacho kiliidhinishwa na mahakama ya Uswidi, kilihusisha wanaume wawili waliochoma moto kurasa za kitabu kitakatifu cha Waislamu nje ya Msikiti Mkuu wa Stockholm siku ya Jumatano. Tukio hilo lilienda sambamba na sikukuu ya Eid al-Adha, sherehe ya Waislamu inayoashiria kumalizika kwa ibada ya Hija ya kila mwaka ambayo huvutia mamilioni ya Waislamu kutoka kote ulimwenguni.

SPA ilisema kuwa mkutano huo utafanyika katika makao makuu ya OIC huko Jeddah na utachunguza "matokeo ya kuchoma nakala ya Qur'ani Tukufu nchini Uswidi katika siku ya kwanza ya Eid Al-Adha".

Ripoti hiyo iliongeza kuwa mkutano wa wiki ijayo utaamua hatua za kuchukuliwa "dhidi ya kitendo hicho kiovu na kuainisha msimamo wa pamoja juu ya hatua zitakazochukuliwa."

Waislamu kutoka kote ulimwenguni wamelaani vikali kitendo hicho kiovu na pia hatua ya serikali ya Uswidi ya kuruhusu uovu huo.

3484145

Kishikizo: oic qurani tukufu uswidi
captcha