Waandamanaji hao ambao akthari yao ni wafuasi wa Muqtada al-Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Al-Sadr ya nchini Iraq mapema leo Alkhamisi wameshambulia malango ya jengo la ubalozi huo wa Uswidi mjini Baghdad huku wakiwa wamebeba Misahafu.
Wamesikika wakipiga nara za kulaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi kwa ridhaa ya serikali. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imewakosoa waandamanaji hao ikisisitiza kuwa, maafisa wote wa ubalozi huo wako salama.
Uswidi imebariki kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa mara nyingine tena, licha ya Waziri wa Sheria wa nchi hiyo hivi karibuni kukiri hadharani madhara ya kiusalama ya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini nchini humo, na akatangaza kwamba sasa serikali ya nchi hiyo imeamua kuchunguza uwezekano wa kuharamisha na kupiga marufuku kuchomwa moto Kitabu hicho kitukufu cha Waislamu.
Ikumbukwe kuwa, Juni 28, Mswidi Salwan Momika mwenye umri wa miaka 37, alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya Msikiti mkuu wa Stockholm, siku ambayo Waislamu Sweden walikuwa katika siku ya kwanza ya Idul Adh’ha.
Mkimbizi huyo wa Iraq aliyepewa uraia wa Uswidi alikivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Waislamu bilioni mbili kwa kibali cha mahakama ya Uswidi na kwa ulinzi kamili wa jeshi la polisi la nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.
Waislamu kote duniani wameendelea kupaza sauti zao kulaani kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Uswidi , huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo ya Magharibi ikishika kasi.
3484417