IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Uswidi yaamua kuzuia maandamano ya kuchoma nakala za Qur'ani Tukufu

18:39 - February 09, 2023
Habari ID: 3476536
TEHRAN (IQNA) - Mamlaka za Uswidi ziliamua kutoruhusu uchomaji moto wa nakala Qur'ani huko Stockholm kwa vile kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu nchini humo kumelaaniwa vikali na ulimwengu wa Kiislamu.

Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yalikuwa yakipanga maandamano, ikiwa ni pamoja na kuchoma Qur'ani Tukufu, siku ya Alhamisi lakini mamlaka za Uswidi zilizuia tukio hilo.

Uamuzi huo ulikuja huku mamlaka ikiamini kuwa hatua kama hiyo inaweza kuharibu ombi la Uswidi la kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO.

Kiongozi wa chama cha siasa chenye misimamo mikali cha Stram Kurs kutoka Denmark, Rasmus Paludan, alichoma nakala ya Qur'ani Tukufu huko Stockholm, Uswidi, Januari 21. Uchomaji moto nakala ya Qur'ani Tukufu ulianzishwa wakati Paludan alipoandamana mbele ya Ubalozi wa Uturuki nchini Sweden kuhusu uanachama wa NATO wa nchi hiyo ya ukanda wa Nordic.

Uswidi na nchi jirani ya Finland zinataka kujiunga na muungano wa kijeshi huku kukiwa na vita nchini Ukraine, na hivyo inajiondoa katika sera ya kihistoria ya kutofungamana na upande wowote.

Hata hivyo, kujiunga kwao kungehitaji idhini kutoka kwa wanachama wote wa NATO, na Uturuki imeonyesha kuwa itazuia jitihada za Uswidi - kwa sehemu kutokana na hatua za  Paludan za kuvunjia heshima Uislamu.

Hata kabla ya hapo, Ankara ilikuwa inashinikiza nchi hizo mbili kukabiliana na makundi yenye silaha ya Kikurdi, ambayo inayaona kama "magaidi".

Wakati huo huo, vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu Ulaya, hasa Uswidi vimelaaniwa vikali na nchi za Kiislamu duniani kote ambazo pia zimeitaka serikali ya Uswidi kuzuia matukio kama hayo.

Aidha kumetolewa miito ya kususia bidhaa za Uswidi na yamkini hatua hiyo pia imechangia nchi hiyo kuzuia vitendo vipya vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kwani bidhaa zake nyingi zinauzwa katika nchi za Kiislamu duniani.

3482410

Habari zinazohusiana
captcha